SALAMU ZA MHE. RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN KWA UONGOZI MPYA KKKT-DAYOSISI MKOANI MARA

Mhe. Prof. John Palamagamba Kabudi Waziri wa Katiba na Sheria akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amempongeza Askofu John Mwita Mwaguge kwa kuwekwa wakfu na kuingizwa kazini kuwa Askofu wa nne KKKT Dayosisi Mkoani Mara siku ya Jumapili tarehe 17/11/2024 Amesema kitendo cha Askofu Maguge kubeba msalaba wakati wa uzinduzi wa Dayosisi hiyo mwaka 1991 ni Ishara kuwa Mungu alimuandaa tangu wakati huo kuja kuwa kiongozi wa Dayosisi na Amemsihi Askofu Maguge kutoionea injili kwamaana mambo yote hayo yametokea kwa neema za Mungu. Akifikisha salamu za Mhe. Rais Samia, Prof. Kabudi amesema Rais amemshukuru Mkuu wa KKKT kwa kumwalika kuwa mgeni rasmi katika Ibada hiyo muhimu na ametoa salamu za pongezi kwa Askofu Michael Adamu kwa kustaafu baada ya kumtumikia Mungu kwa muda wa miaka 15 katika nafasi ya Uaskofu. Prof. Kabudi amesema kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia amewapongeza pia wachungaji na waumini wa Dayosisi hiyo na kuwataka kumpa ushirikiano Askofu Maguge na wasiwe miiba au vikwazo katika uongozi wake. Ameongeza kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa KKKT katika sekta ya elimu, afya, mawasiliano na miundombinu katika kuwasaidia watu wahitaji katika maeneo mengi nchini. Amelipongeza pia Kanisa kwa kutoa mchango mkubwa kupitia vyombo vyake vya habari ikiwemo Television, Magazeti, Mitandao ya Kijamii ambapo vimekuwa na mchango mkubwa katika kuelimisha jamii kupitia mafundisho mbalimbali yanayotolewa kupitia vyombo hivyo. Prof. kabudi amesema Serikali inaahidi kutoa ushirikiano kuhakikisha huduma za Kiroho na kijamii zinazofanywa na KKKT katika kuwahudumia watu wote na kufanikisha malengo yote Kanisa lililoweka yanafanikiwa kwa wakati. Aidha, Kanisa limeombwa kuunga mkono juhudi mbalimbali za kimaendeleo zinazofanywa na Serikali katika kuwahudumia jamii ya watanzania.