CHUO CHA KILUTHERI NYAKATO KUSHIRIKIANA NA CHUO KIKUU CHA IRINGA KUTOA KOZI YA MAENDELEO YA JAMII Askofu wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki Ziwa Victoria Askofu Oscar Itael Lema amesema ushirikiano wao na Chuo Kikuu cha Iringa utaongeza ubora wa utoaji mafunzo kwa wanafunzi wa Chuo cha Kilutheri Nyakato kilichopo jijini Mwanza. Askofu Lema ameyasema hayo jijini Mwanza wakati akifungua kozi ya maendeleo ya jamii katika Chuo cha Kilutheri Nyakato hafla hiyo imeshuhudiwa na uongozi wa Chuo Kikuu cha Iringa, viongozi mbalimbali DMZV, Wachungaji, ,Uongozi wa Chuo cha Kilutheri Nyakato pamoja na wanachuo. Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Magharibi kutoka Kigoma Askofu Jackson Mshendwa amesema kuzinduliwa kwa kozi hiyo kutasaidia kuzalisha wataalamu wengi watakao lisaidia taifa. Naye makamu Mkuu wa chuo Kikuu cha Iringa Profesa Edward Hoseah amewataka wanafunzi kuwekeza kwenye elimu na sio kusubiri elimu ya bure kwani ulimwengu wa sasa ushapitwa na mambo ya bure huku Mkuu wa Chuo cha Biblia cha Kilutheri Nyakato Mchungaji Mimii Brown akikiri kuwa ushirikiano baina ya vyuo hivyo utaongeza wigo wa taaluma katika Chuo hicho. Kabla ya uzinduzi wa kozi hiyo kumefanyika shughuli mbalimbali ikiwemo Uzinduzi wa Kitabu cha Mafundisho Potoshi, na kanuni za kuepuka mafundisho hayo pamoja Na Kanuni za maadili za kuepuka mafundisho potoshi kwa KKKT-Dayosisi za Kanda ya Ziwa na Magharibi pamoja ufunguzi wa nyumba ya watumishi wa Chuo hicho na upandaji miti ili kuunga jitihada za Serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia Nchi.