KKKT-DMZV YAFANYA MAFUNZO MAALUM KWA WANAHABARI WA KANISA

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi Mashariki ya Ziwa Viktoria (DMZV) Limeendesha mafunzo maalum kwa Wenyeviti wa Habari Mawasiliano na Ukaribishaji wa Kanisa iliyofanyika katika Usharika wa Ebenezer, Pasiansi, jijini Mwanza, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uandishi na utangazaji wa habari za Kikristo ndani ya Dayosisi. Akifungua mafunzo hayo, Mratibu wa Kitengo cha Habari Mawasiliano na Ukaribishaji (DMZV) Bi. Pendo Leah Bomani alisema kuwa lengo ni kuongeza ujuzi wa kitendaji ili kuhakikisha habari za Kanisa zinaandikwa kwa weledi, kwa kufuata maadili, na kwa kutumia kanuni za uandishi zinazotambulika kitaaluma. “Tunataka wanahabari wetu wawe na uwezo wa kutoa taarifa sahihi, zinazojenga na kuelimisha jamii ya waumini,” alisema Pendo. Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya Habari Mawasiliano na Ukaribishaji(DMZV) Godlisten Kitomari amewaasa Wenyeviti wa habari kusimamia vyema majukumu Yao na kujitoa kwa moyo ili kuhakikisha wanaandaa habari kwa usahihi na kutekekeleza majumu Yao ili kitengo hicho kifikishe habari kwa waumini wote pamoja na kuwakarimu wageni. Mafunzo hayo yaliyofanyika Novemba 15, 2025 yamehudhuriwa na Wenyeviti wa habari wa sharika za majimbo ya Mwanza kati ,Mwanza Mashariki ,Mwanza kusini na Imani Kanisa Kuu , ambapo mada zilizotolewa ni pamoja na majukumu ya wanahabari wa Kanisa, matumizi ya mitandao ya kijamii,maadili ya habari, matumizi ya lugha sanifu, na mbinu za kuripoti matukio ya Kanisa kwa ufanisi na kuwakarimu wageni. Kwa upande wao, washiriki wamesema mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka kutokana na ongezeko la majukumu ya upashanaji habari katika sharika na idara mbalimbali za Kanisa. “Tumejifunza namna ya kuandika habari zinazowaheshimu waumini na viongozi, bila kupotosha wala kuongeza taarifa zisizo rasmi na tunawaomba Wachungaji wetu na viongozi wengine watupe ushirikiano na watushirikishe vyema ili tuweze kutimiza wajibu wetu kwenye Kanisa ,” alisema mmoja wa washiriki. Mafunzo hayo yanatarajiwa kuendelea kutolewa mara kwa mara kwa Majimbo yote ya Dayosisi huku DMZV ikijipanga kuimarisha dawati la habari ili kuongeza ubora wa taarifa na uwajibikaji katika Kanisa. Mafunzo haya yameambatana na kuwaomba washarika wote kufuata (follow) mitandao ya kijamii ya Dayosisi ambayo ni INSTAGRAM - elctelvd Facebook - ELCT-ELVD