WARATIBU wa Idara za Mawasiliano wa Dayosisi za Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wamekutana mjini Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mafunzo ya pmaoja ya uandishi na utoaji habari za Kanisa pamoja na elimu juu ya mabadiliko ya Tabia ya Nchi. Akifungua mafunzo hayo Naibu Katibu Mkuu Misioni na Uinjilisti kutoka KKKT makao makuu Mchg. Godfrey Walalaze amesema kwamba kukutana kwa waratibu hao ni njia ya kuwaimarisha na kujenga misingi imara ya utoaji wa habari za Kanisa ili ziwafikie washarika wote na jamii kwa ujumla. Kwa upande wake mtoa mada katika mafunzo hayo MCHG. HASBORN MYENDA kutoka KKKT – Dayosisi ya Iringa (DIRA) amesema Kanisa linao wajibu mkubwa katika kuheshimu na kutunza mazingira kwa sababu kutunza mazingira ni kutunza uumbaji wa Mungu na mabadiliko ya tabia ya nchi siyo suala la kisayansi pekee bali ni wito wa kiimani ambao unawahimiza Wakristo kuchukua hatua. Mafunzo hayo yamefanyika kwa siku mbili katika hoteli ya Lutheran Uhuru Mjini Moshi na yamehusisha Waratibu kutoka katika Dayosisi 24 kati ya Dayosisi 28 za KKKT na yanaongozwa na kauli mbiu kutoka kitabu cha Maombolezo 5:4 “Tumekunywa maji yetu kwa fedha; Kuni zetu twauziwa.” Kwa upande wa Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria DMZV imewakilishwa na Mwenyekiti wa Habari na mawasiliano wa DMZV Godlisten Kitomari pamoja na Brenda Makuri kutoka kitengo cha Mawasiliano DMZV.